Ziara ya kukagua hali ya Mitihani ya kidato cha sita

Sat, Aug/22, 2020 Slide-show

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amefanya ziara katika Skuli za Unguja kwa ajili ya kukagua hali ya Mitihani ya Taifa ya kidato cha sita ilivyoanza.

Katika ziara hiyo Mhe Riziki amepata nafasi ya kuzungumza na Wanafunzi ambapo amewataka Wanafunzi watahiniwa, kuepukana na udanganyifu wa aina yoyote wanapokuwa katika mitihani yao.

Amesema kujiamini wakati wa kufanya Mitihani ndio njia pekee itakayowasaidia kujibu vyema Mitihani yao na kuweza kupata ufaulu wa daraja la juu.

Mhe Riziki amewataka Wanafunzi kuhakikisha wanasoma maelezo ya Mtihani unavyoelekeza vizuri kabla ya kujibu maswali ili waweze kujibu majibu ya uhakika kwa kile walichoulizwa.

Aidha Mhe Waziri amesema ni lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu kuondosha kabisa zero na kupunguza alama za daraja la nne ili Taifa lizalishe wataalam mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mwalimu msimamizi wa Mitihani katika Skuli ya Dk Ali Mohamed Shein iliopo Mwembeladu, Meja Mstaafu Zagu Haji Zagu amempongeza Waziri wa Elimu kwa utaratibu aliojiwekea kuhakikisha anapita katika Skuli kuhamasisha Wanafunzi kufanya vizuri katika Mitihani yao,hali hiyo itawapa moya Wanafunzi na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Nae mwanafunzi Amne Pembe Ali kwa niaba ya Wanafunzi wenziwe alimuhakikishia Mhe Riziki kuwa pamoja na kupitia wakati mgumu wa kufungwa Skuli kutokana na maradhi ya covid 19 lakini watafanya vizuri katika Mitihani yao na kufaulu daraja la kwanza.

Katika ziara hiyo Waziri alipata nafasi ya kukagua katika Skuli ya Lumumba, Jang'ombe, Haile sselassie, Hamamni na Kiponda, ambapo jumla ya Wanafunzi 2686 wa kidato cha sita kwa Skuli za Zanzibar wameanza Mitihani yao leo.