kuvunjwa Bodi ya Taasisi ya Elimu

Sat, Aug/20, 2020 Slide-show

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma ameitaka bodi ya ushauri ya Taasisi ya Elimu Zanzibar kuhakikisha inaendelea kutunza siri za kazi zao ili kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kuimarika katika Taasisi zao.

Akizungumza wakati akivunja bodi iliyomaliza muda wake na kuzindua bodi mpya ya Taasisi hiyo, katika ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mazizini mjini Unguja, Mhe Riziki amesema ni lazima kuhakikisha wanalinda dhamana walizopewa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Mhe Riziki pia amewataka kuhakikisha wanashirikiana vyema katika kuimarisha Taasisi ya Elimu, kwa kubuni njia mbadala zikazowezesha kukua zaidi kwa Taasisi hiyo.

Aidha amewataka wajumbe wa bodi hiyo na wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu Zanzibar kuhakikisha wanaweka uzalendo mbele katika nchi na kutochanganya masuala ya kazi na siasa kwani yanaweza kuiharibu kazi yao hiyo.

Amesema hivi sasa ni wakati wa uchaguzi, hivyo ni vyema kuwa makini wakati wa kampeni unapofika, kwa kutoacha kazi na kushughulikia kampeni na hivyo ni vyema kwa anaehitaji kufanya hivyo, kuwa na mawasiliano mazuri na kufuata utaratibu ili kila upande usiweze kuharibikiwa.

Hata hivyo mhe Riziki ameipongeza bodi iliyomaliza muda wake kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuhakikisha kazi za Taasisi hiyo zinakwenda vizuri kwa kuwawekea mazingira mazuri ya utendaji wa kazi zao, ambapo amesema ana imani kuwa kurejeshwa kwao tena katika bodi hiyo wataendeleza mazuri zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti aliemaliza muda wake na kurudishwa tena, dkt Abdullah Ismail Kanduru, amesema haikuwa rahisi kufanya kazi yao kwa pamoja kutokana na ujuzi wa kila mjumbe wa bodi, lakini anashukuru kutokana na hekima na busara za wajumbe na uelewa wamekuwa wakishirikiana na kukubali kukosoana na hatimae wameweza kupata mafanikio mazuri.

Ameahidi kuendeleza jitihada hizo na kurekebisha kasoro walizoziacha ili waweze kufikia malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo.

Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Zanzibar mwalimu Suleiman Yahya Amesema Taasisi hiyo imepata mafanikio mengi ikiwemo kupatiwa ofisi ili kupunguza ufinyu wa nafasi pamoja na kuongezewa bajeti ya Taasisi hiyo.

Aidha ameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa jitihada kubwa inazozichukua kuhakikisha imepata hati miliki ya eneo la Wizara ambalo wanatarajia kujenga jengo jengine jipya mda mfupi ujao.

Bodi mpya ya Taasisi ya Elimu Zanzibar imeundwa ikiwa na wajumbe wanane chini ya Mwenyekiti wake dkt Abdullah Ismail kanduru, ambayo itadumu kwa muda wa miaka mitatu.