Ufunguzi wa Wiki ya Elimu ya Juu

Sat, Aug/19, 2020 Slide-show

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amewataka Wanafunzi wanaotarajia kujiunga na Elimu ya Juu kuitumia vizuri fursa walioipata ya Wiki ya Elimu ya Juu kwa kuweza kujifunza namna ya udahili wa Vyuo vikuu unavyofanyika.

Akizungumza wakati akilifungua Juma la Wiki ya Elimu ya Juu, katika viwanja vya Mapinduzi Square Kisonge amesema iwapo Wanafunzi watapata taaluma nzuri ya kujiunga na Vyuo Vikuu itaondoa tatizo la usajili wa Wanafunzi ambao hawana sifa za kujiunga na vyuo.

Ameeleza kuwa hali hiyo pia itasaidia Wanafunzi kuweza kujua Vyuo ambavyo vimesajiliwa na vinatambulika kisheria kupitia Bodi za usaji wa Vyuo Vikuu, TCU na NACTE.

Aidha amefahamisha kuwa kupitia Juma hilo la Elimu ya juu, wanafunzi wataweza kufahamu namna ya kupata mikopo na masharti yake kwa wale wanaohitaji kuendelea na masomo ambao hawana uwezo wakujisomesha.

Aidha amewataka kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kutokana na taaluma waliyoipata kuwahamasisha na wengine ili lengo la kutoa Elimu hiyo liweze kufikiwa.

Katika Juma hilo, Mhe Riziki alipata nafasi ya kuwapongeza wafadhili mbalimbali waliojitokeza kuchangia kufanikisha shughuli hiyo na kuwaomba kuendelea kutoa kwa lengo la kusaidia harakati za kielimu hapa nchini.

Nae Naibu Katibu Mkuu Taaluma Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bi Madina Mjaka Mwinyi amewasisitiza Wanafunzi kuitumia vyema fursa hiyo ili waweze kupata Elimu kuhusu Taasisi za Elimu ya Juu na kuweza kujua fani zinazotolewa katika vyuo mbali mbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia Bi Aida Juma Maoulid amesema kuwa kupitia Tamasha hilo Wanafunzi watafahamu namna ya kufanya udahili wa kujiunga katika Vyuo pamoja na njia sahihi za kuweza kupata mikopo ili waweze kujiunga na Elimu ya juu.

Akitoa salamu kwa niaba ya Wafadhili wa Juma hilo la Elimu ya juu, mwakilishi kutoka benki ya CRDB amesema kuwa benki yao pamoja na wafadhili wengine watazidi kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ili kuendeleza sekta ya elimu nchini.

Ameeleza kuwa benki ya CRDB imerahisisha upatikanaji wa fedha za mkopo kwa Wanafunzi waliofaidika na Mkopo wa Elimu ya Juu wa Tanzania kwa lengo la kuwarahisishia Wanafunzi kuweza kupata fedha zao kwa wakati na kuwafanya wasome kwa amani wakiwa Vyuoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU prophesa Kihampa amesema wamefarajika kuona muitikio mkubwa wa Wanafunzi katika kupata Elimu ya udahili, ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar katika kutoa Elimu hiyo mara kwa mara ili kuwasaidia Wanafunzi wa Zanzibar kujiunga kwa wingi katika Vyuo vikuu.

Maonesho ya juma la Wiki ya Elimu ya Juu yamefanyika kupitia wazo la mhe Riziki Pembe Juma kwa lengo la kutoa Elimu kwa Wanafunzi waliomaliza masomo ya kidatu cha sita, kujua namna ya kujiunga na Vyuo vikuu, ambayo yatarajiwa kufungwa tarehe 30 Julai, 2020 katika viwanja vya Mapinduzi Square kisonge Mjini Unguja.